Kama Huna Mtaji Na Unahitaji Kuwekeza, Fanya Hivi Kwanza…
Kama Huna Mtaji Na Unahitaji Kuwekeza, Fanya Hivi Kwanza…
Unapokuwa na kiasi fulani cha pesa, na unataka pesa hizo ziongozeke, sina shaka kitu pekee ambacho unachotakiwa kufanya ni kuwekeza pesa hizo ili zikuletee matokeo unayoyataka. Kwa kuwekeza pesa hizo itakusaidia kujenga uchumi imara wa kipesa.
Halikadhalika, unapokuwa hauna pesa, kitu gani unachotakiwa kufanya? Pia hapa, unatakiwa kuwekeza vizuri katika rasilimali ulizonazo kama muda wako, kipaji chako, maarifa, uzoefu wako na hata nguvu ulizonazo.
Kama wenye pesa wanavyowekeza, pia kama huna kitu unatakiwa kuwekeza katika rasilimali hizo za msingi ili kujenga msingi mkubwa wa mafanikio yako kesho. Hutakiwi kulia eti huna pesa, wekeza katika vile ulivyonavyo ndani mwako kwanza.
Pia unaweza ukajiuliza nitawekeza vipi wakati sina pesa, sikiliza kuwekeza katika maisha yako haimaanishi kila wakati lazima ukawa unapesa, anza kuwekeza na yale mambo ambayo yatakupa faida kesho. Kivipi hili linawekana? Sikiliza.
Kwa kadri unavyojifunza hapo unakuwa unatengeneza thamani kubwa sana kwako itakayokuingizia kipato. Hakuna maarifa ambayo yanatumiwa vizuri yanamwangusha mtu, tumia muda wako kujifunza utaona matokeo bora sana kwako.Anza kuwekeza kwenye muda wako, kwa kuwa sasa hivi pengine hauna kitu cha kufanya, muda wako wekeza kwa kujifunza katika mambo mbalimbali. Wekeza muda wako kujifunza juu ya mafanikio au chochote ukitakacho.
Anza kuwekeza kwenye nguvu zako, hakuna mtu ambaye amezaliwa hana nguvu. Kila mtu ana nguvu fulani, kwa kuwa huna mtaji na huna kiato cha uhakika hebu zitumie nguvu zako zikusaidie kukuingizia pesa zitakazokusaidaia kukutoa hapo ulipo.
Tumia nguvu zako kwenye kilimo, tumia nguvu zako kwenye kubeba mizigo, tumia nguvu zako kwenye chochote kile unachoweza ili ziwe na manufaa kwako. Hujapewa hizo nguvu zako bure, zifanyie kazi.
Anza kuwekeza kwenye vipaji vyako, kaa chini ujiulize una kitu gani cha thamani ambacho ukikitumia kinaweza kukusaidia kufanikiwa? Kama ni kuchora, chora kweli, kama ni kuimba, imba kweli, kipaji chochote ulichonacho kitumie.
Wengi wanaojua kutumia vipaji vile walivyonavyo wanafanikiwa sana, nawe pia unaweza kuwa miongoni mwao. Kitu kikubwa unachotakiwa kujua, usijidharau, jiamini na kisha tafuta kipaji chako na kitumie mara moja.
Anza kuwekeza kwenye uzoefu na maarifa ulionayo, tumia uzoefu wako na maarifa hata kama ni kidogo kutafuta fursa za kibiashara. Unaweza kuwashirikisha watu wengine wazo ulilonalo na ikakusaidia kupata mtaji na hatimaye kufanikiwa.
Hapa kwa kifupi namaanisha unaweza kuwa mtu wa kati, yaani kutafuta fursa na kumshirikisha yule mwenye pesa au uhitaji na yeye akakulipa. Huhitaji kuona haya kwenye maisha, vinginevyo utaumbuka.
Kwa hiyo mpaka hapo unaona ili kufanikiwa kila mtu anahitaji kuwekeza. Mwenye pesa anahitaji kuwekeza pesa zake sana na hata pia na wewe ambaye hauna pesa unahitaji kuwekeza vile vitu vya msingi ulivyonavyo.
Usijidanganye kuanza kuangalia ‘season movies’ usiku na mchana kwa kuwa eti bado hujaajiriwa na serikali au huna kitu cha kufanya. Nikupe uhakika kama unafanya hivyo basi umeamua kupoteza maisha yako mwenyewe tena kwa hiari yako.
Kumbuka hitaji la kuwekeza kila siku kila mtu analo bila kujali mtu huyo ni maskini au tajiri.
Maoni
Chapisha Maoni